Maendeleo ZBS yamkosha bosi ARSO

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 06:01 AM Apr 17 2024
Katibu Mkuu wa Shirika la Viwango Afrika (ARSO), Dk. Hermogene Nsengimana.
Picha: Maktaba
Katibu Mkuu wa Shirika la Viwango Afrika (ARSO), Dk. Hermogene Nsengimana.

KATIBU Mkuu wa Shirika la Viwango Afrika (ARSO), Dk. Hermogene Nsengimana ameridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) toka ilipojiunga na shirika hilo kama mwanachama mwangalizi.

Dk. Nsengimana alisema hayo juzi alipotembelea ofisi za taasisi hiyo zilizopo Maruhubi na kukagua baadhi ya maabara pamoja na kuzungumza na uongozi wa taasisi hiyo.

Dk. Nsengimana amefanya ziara hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake nchini kukagua maandalizi ya mkutano mkuu wa mashirika ya viwango Afrika unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Alisema kuwa taasisi hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuongeza idadi ya maabara na kuweka mifumo imara ya ukaguzi kiasi cha maabara ya uchunguzi wa bidhaa za kemikali kupata alama ya ithibati ya taassi ya udhibiti ubora kwa nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika.

“Nimefurahi kuona ZBS inaendelea kuimarika na kuna ongezeko la maabara. Hii ni hatua muhimu kwa taasisi yenye dhamana kubwa kama hii, hivyo ni vyema kama shirika linalosimamia mashirika ya viwango barani Afrika tujivunie hatua iliyofikiwa”, alisema Dk. Nsengimana.

Aidha, aliwataka watendaji wa taasisi hiyo kuendelea kusimamia miongozo na makubaliano ya kikanda na kimataifa wanaposhughulikia uthibitishaji wa viwango wa bidhaa, ili kulinda hadhi ya bidhaa zinazozalishwa au kuingizwa nchini.

Akizungumzia mkutano mkuu wa ARSO, Dk. Nsengimana alisema amefurahishwa kuona kuna ushirikiano katika maandalizi ya mkutano huo kati ya wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zinazosimamia taasisi za viwango nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa ZBS, Yussuph Majid Nassor, alisema wamefarajika kutembelewa na kiongozi huyo ambaye aliambatana na Mratibu wa Miradi wa Shirika hilo, Sandra Umugwaneza.

Alisema taasisi imepata fursa ya kuainisha mambo mbali mbali ambayo yatawasilishwa katika vikao vya ARSO kabla ya mkutano mkuu ambao utafanyika Zanzibar.

Aidha, alisema kuwa ziara ya kiongozi huyo iliyoanzia Tanzania Bara kwa kukutana na viongozi mbalimbali wakiwemo wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imekuja wakati muafaka ambapo taasisi hiyo ipo katika mchakato wa kukamilisha maabara tano mpya ikiwemo ya bidhaa za ujenzi.