Mtanzania Ashinda Tuzo ya Global Citizen mwaka 2024

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:06 AM Apr 15 2024
Mshindi wa Tuzo ya Shirika la Kimataifa la Global Citizen kwa mwaka 2024, Lydia Moyo, akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mshindi wa Tuzo ya Shirika la Kimataifa la Global Citizen kwa mwaka 2024, Lydia Moyo, akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

MTANZANIA Lydia Charles Moyo, amekuwa mmoja kati ya washindi sita waliotambuliwa kwa Tuzo ya Shirika la Kimataifa la Global Citizen mwaka 2024, ikionyesha juhudi za vijana ulimwenguni katika kuleta mabadiliko.

Kwa mujibu wa taarifa, uthabiti wake usio na kifani katika kukabiliana na umasikini na kuwezesha kiuchumi kwa wasichana na wanawake vijana ndiyo umeleta utambuzi huu wenye heshima duniani, na kumweka pamoja na kikundi cha vijana wachache kinachong'ara miongoni mwa mamilioni ulimwenguni kote.

Hata hivyo, kwa mujibu wa tovuti ya Shirika la Her Initiative, ambalo Lydia ni Mkurugenzi na mwanzilishi wake, lilianzishwa miaka mitano iliyopita ambapo kupitia shirika hilo linaloongozwa na wanawake vijana, Lydia hutekeleza miradi inayolenga kuwawezesha kifedha wasichana na wanawake vijana, kuchagiza matumaini na fursa mahali ambapo wasichana na wanawake wamekata tamaa.

Akizungumzia utambuzi huo, Lydia ameishukuru timu ya Her Initiative, washirika, wafadhili, na wafuasi wa kazi zake, wote wa ndani ya Tanzania na kimataifa. "Tuzo hii inamaanisha mengi kwangu na kazi tunayofanya na Shirika la Her Initiative. Inathibitisha uimara na azimio la wanawake na wasichana vijana, ambao wana ndoto na malengo makubwa na wanafanya kazi kwa bidii ili kuboresha si tu maisha yao binafsi, bali pia ya jamii zao," alisema na kuongeza. 

"Napenda pia kutambua juhudi za watu binafsi na mashirika yote, ndani na nje ya Tanzania, ambao wametoa mchango mkubwa." 

Akizungumzia ombwe kubwa la kijinsia katika upatikanaji wa uchumi, Lydia alisisitiza umuhimu wa kazi wanayofanya na Her Initiative. Kwa kutumia mikakati na mbinu mbalimbali za uwezeshaji kiuchumi na kwamba Her Initiative wanakusudia kuvunja mzunguko endelevu wa umaskini na kuimarisha uwezo wa kiuchumi kwa wasichana na wanawake vijana wa Kitanzania.

Alisema kiini cha mikakati yao ni uwezeshaji kiuchumi na uvumbuzi wa kiteknolojia, kama ilivyoonyeshwa na jukwaa la kielimu la 'Panda Digital' ambalo  ni la kujifunza mtandaoni linalotumia kiswahili na tayari limewawezesha zaidi ya wasichana na wanawake 5,000 kote Tanzania kupata ujuzi muhimu wa masoko na biashara, huku pia likiwawezesha kuunganishwa na fursa na mtandao muhimu kuanzisha na kukuza biashara zao.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyochapishwa na Global Citizen, Liza Henshaw, Rais wa Global Citizen, amesisitiza jukumu muhimu la uongozi wa vijana katika kuleta mabadiliko halisi. 

Anna Kulaya ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Shirika la Her Initiative, alisema hamasa ya Lydia haina ufananisho na dunia inapaswa kuwaunga mkono viongozi wanawake wenye uthubutu kama yeye. 

Washindi wa Tuzo ya Global Citizen mwaka 2024 watatambuliwa wakati wa mkutano wa ‘Global Citizen NOW’ hapo Mei Mosi na 2, mwaka huu huko New York, Marekani. 

Global Citizen ni Shirika la Utetezi na Uchechemuzi la Kimataifa linalopigania kumaliza umaskini. Kwa msaada wa jamii ya kimataifa ya watetezi wa kila siku wanaopaza sauti zao na kuchukua hatua, juhudi zao zinapata nguvu kupitia kampeni na matukio yanayokusanya viongozi katika muziki, burudani, sera za umma, vyombo vya habari, hisani, na sekta ya biashara.

Katika kipindi cha muongo mmoja, Global Citizen imefanikisha ahadi za zaidi ya dola bilioni 43.6, ikichochea miradi ya mageuzi ambayo imegusa maisha ya watu takriban bilioni 1.3 ulimwenguni. Mafanikio haya yanathibitisha nia ya shirika hilo kutimiza ulimwengu usio na umaskini, huku likiashiria nguvu ya hatua ya pamoja katika kuendesha maendeleo kwa kiwango cha kimataifa.