TPA yaendelea kung’ara hati safi za ukaguzi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:54 AM Apr 16 2024
Bandari ya Dar es Salaam.
Picha: Maktaba
Bandari ya Dar es Salaam.

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imesema imeongeza ufanisi katika uandaaji na utoaji wa taarifa za hesabu za Mamlaka na kufanikiwa kupata hati safi kwa miaka miwili mfululizo.

Mafanikio hayo yamekuja baada ya mamlaka hiyo kukamilisha mradi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ambao hutumika katika kuandaa na kuhifadhi taarifa za kifedha.

Katika taarifa yake jana, Mamlaka hiyo ilisema kaguzi zilizofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kwa miaka mfululizo miwili iliyopita  ndiko kumeiipata mamlaka hiyo hati safi.

Ilisema TPA chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu wake, Plasduce Mbossa,  imefanikiwa kutekeleza kwa mafanikio makubwa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa na mifumo Madhubuti ya TEHAMA inatumika. 

Ilisema katika  mwaka wa fedha 2022/2023 miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na utekelezaji wa maagizo ya Rais ya  kukamilisha mradi wa TEHAMA  ambao hutumika katika kuandaa na kuhifadhi taarifa za kifedha. 

Ilisema mfumo huo pia huunganisha shughuli za Idara mbalimbali katika kutekeleza majukumu ya kila siku na kwamba unaunganisha Idara zote muhimu kama Idara ya Fedha, Idara ya Rasilimali watu, Idara ya manunuzi na nyinginezo. 

“Matokeo ya kukamilika kwa mfumo huu, ni sanjari na ufanisi katika uandaaji na utoaji wa taarifa za hesabu za TPA, ambapo mfumo huo umeiwezesha TPA kupata hati safi kwa miaka miwili mfululizo kwa kaguzi zinazofanywa na (CAG),” ilisema.

Aidha, taarifa hiyo ilisema kutokana na matumizi ya mfumo huo, TPA imeweza kupata tuzo ya uandaaji bora wa taarifa za hesabu kutoka kwa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu, NBAA. 

Ilisema zaidi ya hayo, mfumo huo umeongeza tija pia katika kuhakikisha udhibiti wa mianya ya upotevu wa fedha, uandaaji wa taarifa mbalimbali kwa wakati, utunzaji wa nyaraka na taarifa za kifedha na rasilimali za taasisi. 

 Kutokana na kuimarika mifumo ya ukusanyaji mapato imesababisha mapato ya TPA kuongezeka kwa asilimia 27 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2021/2022.

Ilisema kwa upande wa kuhudumia shehena kumekuwa na ongezeko kubwa kwa upande wa meli na shehena ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 idadi ya Meli zilizohudumiwa na Bandari za TPA ziliongezeka na kufikia meli 4,762 kutoka meli 4,160 ambazo ni wastani wa ongezeko la asilimia 13.9 kwa mwaka. 

Ilisema kwa upande wa shehena kiwango cha shehena kilichohudumiwa ni tani milioni 27.8 sawa na wastani wa ongezeko la asilimia 21.7 ya shehena iliyohudumiwa katika mwaka husika ukilinganisha na miaka ya nyuma. 

Aidha, ilisema kwa upande wa miundombinu, Mamlaka imefanya uboreshaji   mkubwa wa miundombinu ikiwemo uundwaji wa mifumo ya TEHAMA, Utekelezaji wa Mradi wa Kimkakati wa Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam (DMGP), Uboreshaji wa Bandari Tanga, Upanuzi wa Bandari ya Mtwara, Uboreshaji wa Bandari za Maziwa Makuu.

Ilisema uwekezaji huo mkubwa na ununuzi wa mitambo pamoja na ujuzi kwa wafanyakazi umeongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa Mamlaka ya Bandari kwenye bandari zake zote nchini.