Ulega ataja mafanikio miaka 60 ya muungano mifugo, uvuvi

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 06:43 AM Apr 17 2024
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ametaja mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya muungano mojawapo ni kuandaa mradi mkubwa wa miaka mitano utakaogharimu Dola za Marekani milioni 117, unaolenga kuleta mageuzi kwenye sekta ya uvuvi na ufugaji samaki.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa kuhusu ushirikiano wa Tanzania Bara na Zanzibar kwa miaka 60 katika sekta ya mifugo na uvuvi, Ulega alisema fedha hizo ni mkopo na utekelezaji wake utaanza kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Alibainisha kuwa mradi huo umeandaliwa kwa pamoja kwa kushirikiana na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar.

Alifafanua kati ya fedha hizo kiasi kitakachotumika kwa Tanzania Bara ni Dola za Marekani milioni 65, Zanzibar ni Dola za Marekani milioni 41 na Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu itapatiwa Dola za Marekani milioni 10. 

Kuhusu mwani, Waziri Ulega alisema serikali imeendelea kuimarisha zao hilo katika pande zote za Muungano ambapo kwa mwaka wa fedha uliopita zaidi ya Sh.milioni 400 zimetolewa kwa ajili ya kuongeza chachu ya kilimo hicho kwa wanawake.

Alisema hadi sasa tani 5,000 zinazalishwa Tanzania Bara na wataalamu wameanza kufanya utafiti ili mwani utumike kutengeneza bidhaa za chakula cha mifugo kutokana na kuwa na virutubisho vya kutosha.

Kuhusu sekta ya mifugo, Ulega alisema kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kuimarisha diplomasia, nyama tani 35,297 zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 146.43 zimeuzwa nje ya nchi.