Wafanyabiashara watakiwa kuwalinda walaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:42 PM Apr 16 2024
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Frank Mmbando.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Frank Mmbando.

BARAZA la Ushindani (FCT) limewataka wafanyabiashara kuzingatia misingi halali na kumlinda mnunuzi wa mwisho ili kupunguza malalamiko na migogoro baina yao.

FCT mwishoni mwa wiki iliyopita iliendesha mafunzo kwa wadau wake, wakiwemo wafanyabishara ili kupata uelewa utakaowasaidia kujua haki na wajibu wao ikiwemo kumlinda mlaji katika soko.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Frank Mmbando, alisema mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza ufanisi kwenye uzalishaji ikiwa ni pamoja na usambazaji na utoaji wa huduma kwa jamii.

“Baraza limefanya jambo la muhimu sana elimu watakayoipata ni muhimu sana kwani itasaidia kutambua haki na wajibu, kustawisha ushindani, na kuongeza kasi ya uwajibikaji katika soko na kusaidia kutatua migogoro ya kiushindani baina ya wadau,” alisema Mmbando
Aliwataka washiriki hao kutumia vizuri baraza hilo kutatua changamoto za biashara zinazoweza kujitokeza kwani ni chombo kinachosimamia haki kwa watu wote.

Ofisa Sheria Mkuu wa FCT, Hasfa Said, alisema kati ya kazi zinazofanywa na baraza hilo ni kupokea, kusikiliza na kuamua rufaa zinazotokana na maamuzi ya mamlaka za usimamizi na udhibiti pamoja na tume hiyo ya ushindani.

Alisema baraza hilo linatekeleza sheria ya ushindani ya Bunge na kanuni zake za mwaka 2012.

Aliwataka wafanyabiashara kutumia baraza  hilo kwa ajili ya kuwalinda walaji na kuhakikisha wanapata ufanisi katika soko na kukuza uchumi wa nchi.

Mkuu wa Idara ya Uchumi wa FCT, Kulwa Msogoti, alisema baraza hilo linahamasisha wafanyabiashara,  wawekezaji,  watoa huduma  na walaji kupeleka malalamikom kama hawajaridhika na maamuzi  yanayotolewa na Tume ya Ushindani na vyombo  vya udhibiti.
 
Alisema baraza hilo linawahamasisha wadau wote  wanapodai haki wanatakiwa kutumiza wajibu wao na kufuata sheria za nchi hususani  katika  biasha na udhibiti wa soko. 

Mwenyekiti wa Daladala wa Jiji la Arusha, Maulid Abdallah, alisema kuna mambo mazuri yameelezwa na baraza hilo ikiwemo haki kumlinda mlaji  utaratibu wa kuendesha uchumi  wa nchi kwa sekta mbalimbali.

Ofisa Mdhibiti Ubora wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA), Dismoso Chimbunde, alisema lengo la kuhudhuria mafunzo hayo ni kufahamu namna gani ya kukuza na kuwaendeleza wafanyabiashara nchini.

 Kaimu Ofisa Huduma kwa Wateja na Utawala wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Sharifa Lengima, alisema wamekuwa wakijitahidi kutetea haki za watumiaji  wa huduma za nishati na maji.