Wajasiriamali Kahama wapata mafunzo uzalishaji bidhaa bora

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 08:19 PM Apr 15 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita (wa kwanza kulia), akifungua mafunzo ya Wajasiriamali Kahama.
Picha: Shaban Njia
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita (wa kwanza kulia), akifungua mafunzo ya Wajasiriamali Kahama.

WAJASIRIAMALI wanaojishughulisha na uzalishaji, usindikaji na ufungashaji bidhaa za uokaji kutoka Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, wamenufaika na elimu ya utengezaji bidhaa zenye ubora utakao wawezesha kupata nembo ya shirika la viwango nchini (TBS).

Akitoa taarifa ya mafunzo haya leo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mboni Mhita, Meneja wa Mafunzo na Utafiti wa TBS Kanda ya Ziwa, Hamisi Sudi amesema, wajasariamali wengi wanazalisha bidhaa nyingi lakini hazina ubora.

Sudi anaamini kuwa kutokuwa na ubora unaohitajika ni chanzo cha wao kukosa nembo ya ubora kutoka TBS, na hivyo kuzifanya bidhaa zao kushindwa kushinda katika soko la ndani na nje.

Amesema mafunzo hayo yamewanufaisha wajasiriamali 35 wenye kuzalisha bidhaa mbalimbali, na kwamba mada zilizotolewa ni pamoja na soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki, viwango, faida na matakwa ya viwango katika bidhaa za uokaji.

Mada nyingine kwa mujibu wa Sudi ni pamoja na usajili wa biashara, kanuni bora za usindikaji (GMP) na utaratibu wa uthibitishaji wa ubora wa bidhaa.

Aidha, wajasiriamali hao pia wamepata elimu kuhusu usajili wa majengo na bidhaa za chakula, usafirishaji bidhaa nje ya nchi (TAE), kanuni bora za usafi (GHP), teknolojia za usindikaji wa bidhaa za uokaji, vifungashio, ufungaji na fursa za ofisi ya maendeleo ya jamii.

Awali akifungua mafunzo hayo, DC Mhita ameitaka TBS kuongeza wigo wa kuwafikia na kuwaelimisha wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo, ili mwisho wa siku siyo tu kuwa na bidhaa bora zenye kushindana ndani na nje, lakini pia zisimuathiri mtumiaji wa mwisho.

Amesema, mahali ambapo kulikuwa na mgodi wa Barrick Buzwagi, sasa eneo hilo ni kituo maalumu cha uwekezaji, na kwamba kuna kampuni nyingi zinakuja kuwekeza, hivyo bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali hao zitapata soko la uhakika, muhimu ziwe na ubora.