Kiongozi wa Jeshi Chad achaguliwa kuwa Rais

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:16 AM May 10 2024
Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby.
Picha: Maktaba
Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby.

TUME ya Uchaguzi nchini Chad, imemtangaza Kiongozi wa Jeshi, Mahamat Idriss Deby kuwa Rais baada ya kuibuka mshindi wa awali kwa zaidi ya asilimia 61 ya kura dhidi ya mpinzani wake mkuu Succes Masra ambaye ameonekana kuyapinga matokeo hayo.

Matokeo hayo yaliyokuwa yanatarajiwa Mei 21, yametolewa wiki moja mapema, na yamemuonesha Deby Itno akiwa na asilimia 61 ya kura huku Masra akipata asilimia 18.5 ya kura hizo. Kumesikika milio ya risasi N'djamena baada ya matokeo hayo kutangazwa. 

Utawala wa kijeshi wa Chad umekuwa wa kwanza kati ya nchi zilizokumbwa na mapinduzi katika Afrika Magharibi na Kati kurejesha sheria ya kikatiba kupitia sanduku la kura, lakini baadhi ya vyama vya upinzani vimelalamika kilio chao kuhusiana na wizi wa kura.

Mkuu wa Shirika la Kitaifa la Kusimamia Uchaguzi nchini humo, Ahmed Barticet amesema Deby amepata aslimia 61.3 ya kura bila shida ikiwa ni zaidi ya asilimia 50 inayohitajika ili kuzuia duru ya pili.

Chadi ilifanya uchaguzi wake baada ya kucheleweshwa kwa muda mrefu, huku ikiwa chini ya utawala wa kijeshi kwa miaka mitatu. Wachambuzi wanasema walitarajia ushindi kwa Mahamat Deby Itno ambaye yuko madarakani.