Mambo manane kupaisha sekta ya maji

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 10:45 AM May 10 2024
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

WIZARA ya Maji imeanika vipaumbele vinane kwa mwaka 2024/25 vinavyolenga kuboresha huduma ya maji kwa kusambaza maji safi na salama kwa zaidi ya asilimia 85 ya wakazi wa vijijini na zaidi ya asilimia 95 wa mijini.

Katika kufikia malengo hayo, serikali kupitia Wizara ya Maji, imesema itaongeza  ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji na uendeshaji wa skimu za maji.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25 Waziri wa wizara hiyo, Jumaa Aweso, ameomba Bunge kupitisha Sh. Bilioni 627.78 ili kutekeleza vipaumbele hivyo ambavyo vitazingatia kuimarisha usimamizi, uendelezaji,uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na kuimarisha na kusimamia huduma za ubora wa maji.

Ametaja vipaumbele hivyo kuwa ni kukamilisha utekelezaji wa miradi inayoendelea na kuendelea na ujenzi wa miradi mikubwa, kuongeza kasi ya uvunaji wa maji ya mvua kwa kujenga mabwawa ya ukubwa wa kati na ya kimkakati, kufikisha huduma ya maji kwenye vijiji ambavyo havina huduma,  kukamilisha uandaaji wa Mpango Kabambe wa Taifa wa Maji,  Mtandao wa Taifa wa Kusambaza Maji  na mapitio ya Sera ya Taifa ya Maji.

“Kipaumbele kingine ni kukamilisha na  kupunguza upotevu wa maji, kuongeza kasi ya ufungaji wa dira za malipo kabla ya matumizi ya maji, kuongeza kasi ya uwekezaji kwenye usafi wa mazingira na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji na uendeshaji wa skimu za maji”, amesema Aweso.

Amesema katika mwaka ujao wa fedha, serikali  itakarabati miradi ya maji na kudhibiti wizi wa maji ili kupunguza kiwango cha maji yanayopotea kutoka wastani wa asilimia 35.3 ya maji yanayozalishwa hadi kiwango kinachokubalika kimataifa cha asilimia 20. 

Hali hiyo pia amesema inahusisha ukarabati wa miundombinu ya maji iliyochakaa, kufunga dira za maji ya jumla  na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya maji.

Amesema itaendelea kufanya tathmini na ufuatiliaji wa ubora wa maji katika vyanzo vya maji 2,200, mifumo ya usambazaji maji 8,245 vijijini na mijini na mifumo 150 ya majitaka. 

Pia amesema serikali imepanga kuweka mifumo ya ukusanyaji na utunzaji wa takwimu na taarifa za ubora wa maji; kuendelea kutekeleza mkakati wa kupunguza madini ya flouride kwenye maji ya kunywa na ya kupikia na kuwezesha uandaaji na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango ya usalama wa maji katika mamlaka za maji 40 na CBWSOs 120.

Waziri Aweso amesema serikali itaendelea kuimarisha mfumo wa kufuatilia mwenendo wa rasilimali za maji ikiwemo ukarabati wa vituo 100 vya usimamizi wa rasilimali za maji, kutoa vibali 600 vya matumizi ya maji,  kuunda jumuiya 18 za watumia maji na kuunda kamati tisa  za vidakio vya maji.

Amesema wizara pia itaimarisha uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji kwa kutambua vyanzo vya maji juu ya ardhi na maeneo yenye hifadhi ya maji chini ya ardhi. Na kufanya utafiti wa kina ardhini ili kutambua maeneo yenye maji na kuyafanya kuwa maeneo tengefu ili kuhakikisha usalama wa maji unakuwapo.

“Serikali itaendelea endelea kutekeleza miradi 1,095 ya usambazaji maji vijijini katika maeneo mbalimbali nchini na kuchimba visima vitano  katika kila jimbo la uchaguzi kwenye maeneo ya vijijini ikianza visima 900. Hali hiyo itaongeza upatikanaji huduma ya maji  maji vijijini kutoka wastani wa asilimia 79.6 hadi zaidi  85 ifikapo mwaka 2025,”alisema.

Pia amesema serikali itaendelea kubadili  mitambo inayotumia dizeli na kuweka umeme wa gridi ya taifa au nishati ya jua ili kupunguza gharama za uendeshaji wa skimu za maji na kuimarisha usimamizi wa mauzo ya maji na makusanyo kwenye CBWSOs kwa kufunga mfumo wa  malipo kabla ya matumizi, kuweka mfumo wa pamoja wa ankara za maji na kujiunga kwenye mfumo wa makusanyo ya fedha za umma.

“Wizara kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na sekta binafsi imepanga kutekeleza jumla ya miradi 247 ya maji mijini. Lengo ni kuhakikisha zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wa mijini wanapata huduma ya maji safi na salama ifikapo mwaka 2025,” amesema Aweso.