Samia aagiza kulegezwa masharti uwekezaji

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 10:38 AM May 10 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa ndani ya mojawapo ya Gari lililounganishwa katika Kiwanda cha Kuunganisha Malori na Matipa cha Saturn Corporation Limited kilichopo Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Picha: Maktaba
Rais Samia Suluhu Hassan akiwa ndani ya mojawapo ya Gari lililounganishwa katika Kiwanda cha Kuunganisha Malori na Matipa cha Saturn Corporation Limited kilichopo Kigamboni Jijini Dar es Salaam.

RAIS Samia Suluhu Hassan ameagiza Wizara ya Viwanda na Biashara na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kupunguza urasimu na kulegeza masharti ili kuvutia uwekezaji.

Amesema hatua hiyo itachochea uwekezaji na viwanda kujengwa kwa wingi, hivyo kuongeza ajira na mapato serikalini.

Pia amesema ili kuchochea ukuaji wa viwanda, serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi, itajielekeza kuwezesha kuzalisha viwanda vinavyosaidia vingine na kwamba katika kutekeleza sera ya viwanda, kuna haja waziri kuhakikisha viwanda vinasomana.

Akizungumza Kigamboni, Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kuunganisha magari makubwa ya Howo kinachomilikiwa na kampuni ya Saturn Corparation Limited, amesema amekuwa akizungumzia suala la mifumo kusomana ili kurahisisha ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ya uwekezaji na viwanda.

“Viwanda vitambuane na visomane, nani anamzalishia nini nani, ili tutengeneze ‘block chain’. Lakini pia ni fursa ya kuwa na kongani za viwanda vidogo vingi vitakavyolisha vikubwa ili vizalishe kwa haraka na kwa bei nafuu na tuingie kwenye soko tukiwa washindani wakubwa,” amesema.

 Rais Samia amezielekeza wizara hizo kumaliza haraka suala la mgodi wa Mchuchuma na Liganga ili kupata kampuni nzuri itakayoanza kuchimba chuma ili kitumike kama malighafi katika kiwanda hicho na vingine vitakavyokuwa na uhitaji.

Amesema serikali imeimarisha mazingira ya uwekezaji ikiwamo kupunguza kodi ya kampuni kutoka asilimia 30 hadi 10 kwa kipindi cha miaka mitano ili kuchochea uwekezaji, ajira, na kurahisisha upatikananji wa magari.

Pia amebainisha kuwa anafarijika baada ya kuona kiwanda hicho kimeshatoa ajira za moja kwa moja 250 na zisizo za moja kwa moja takribani 1,800 na kwamba hiyo ni hatua nzuri itakayoongeza mzunguko wa fedha.

“Uamuzi wa kampuni hii utachangia ukuaji wa sekta zingine kama kilimo, madini na usafirishaji kwa kuongeza uwezo na ufanisi wa shughuli za uzalishaji. Pia  kiwanda hiki kitatumia vioo vinavyozalishwa na kiwanda kingine ambacho zaidi ya asilimia 80 ya malighafi zinapatikana nchini,” amesema.

Rais Samia amesema baada ya kuangalia kiwanda hicho, amebaini kuna vitu vingi vinaweza kuzalishwa hapo na kwamba anaendelea kuwavutia wawekezaji kuja kuweka viwanda vingine nchini, huku akimwelekeza Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, kuhakikisha mnyororo huo haukatiki.

“Tuwe na ‘block chain’ kutoka uzalishaji mmoja kwenda mwingine. Kila  mmoja ampe mwenziwe vifaa vya kuzalisha na kwa namna hivyo viwanda vitakuwa vingi, ajira zitakuwa nyingi na mapato kwa serikali yataongezeka pia,” amesema.

Pia amesema amejulishwa kwamba idadi ya vipuri vinavyotumika kuunganisha gari moja katika kiwanda hicho ni takribani 2,400 ambavyo vingi vinatoka nje na kuweka bayana kuwa hiyo si afya kwa ukuaji wa viwanda na anaiona kama fursa kwa Watanzania.

Amesema wanaweza kunufaika zaidi kupitia uwekezaji wa viwanda vingine vya uzalishaji wa vipuri vya magari na mitambo na kwamba kuna malighafi zinazopatikana nchini kikiwamo chuma kilichoko Mchuchuma na Liganga ambacho kinaweza kutumiwa na kiwanda hicho.

Rais amesema jitihada za kuvutia mitaji na uwekezaji nchini ni jambo la kuungwa mkono na kila mmoja na kila mdau ana wajibu wa kuhakikisha uwekezaji unadumu na unakuwa endelevu. 

Serikali kwa upande wake, amesema ina wajibu wa kuendelea kuimarisha mazingira bora na yanayotabirika kufanyia biashara.

Amesema wawekezaji wana wajibu wa kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuwa na bei shindani ndani na nje. Pia alisema wananchi wana wajibu wa kujifunza haraka teknolojia inayoletwa na wawekezaji, kufanya kazi kwa bidiii na kwa uaminifu.

“Tuepuke ruhusa za uongo. Tujenge  utamaduni wa kuthamini kazi zetu. Pia  wananchi kama wanunuzi tuna wajibika kulinda viwanda na uwekezaji unaofanywa nchini kwetu. Tunaponunua bidhaa zinazozalishwa nchini tunawezesha wawekezaji kuongeza uzalishaji na ubora wa bidhaa, kulinda ajira za vijana wetu na kuchangia kuimarisha uchumi wa nchi yetu.

“Kinyume chake ni kwamba tunasafirisha kazi zinakwenda nchi zingine na sisi tunawapelekea malighafi wazalishe, wajenge uchumi wa nchi zao, watengeneze ajira kwa watu wao. Huo mtindo wa uchumi wa aina hiyo tunaupiga marufuku na sasa tunajielekeza kuzalisha ndani,” amesema.

Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Ashatu, amepongeza viongozi na menejimenti ya kiwanda hicho kwa kuwaamini na kuamua kuwekeza nchini, huku akiwatoa wasiwasi kwamba wako pamoja na watashirikiana kila hatua.

Amesema viwanda na biashara ndio msingi wa uchumi wa taifa na kwamba uwekezaji ambao uko juu kwa sasa nchini ni sekta za viwanda na biashara na ndizo zilizoajiri Watanzania wengi kuliko sekta zingine.