TAS walaani mwenzao kushambuliwa

By Enock Charles , Nipashe
Published at 02:03 PM May 10 2024
Baadhi ya Viongozi kutoka Chama cha Wenye Ualbino Tanzania (TAS) wakitoa tamko kuhusu mwenzao kushambuliwa huko mkoani Geita, jijini Dar Salaam.
Picha:Mpigapicha Wetu
Baadhi ya Viongozi kutoka Chama cha Wenye Ualbino Tanzania (TAS) wakitoa tamko kuhusu mwenzao kushambuliwa huko mkoani Geita, jijini Dar Salaam.

CHAMA cha Wenye Ualbino Tanzania (TAS) kimeiomba jamii kuwalinda watu wenye ualbino kueleka kipindi cha uchaguzi na kulaani matukio ya baadhi yao kuvamiwa na kushambuliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam juzi, Msemaji Mkuu wa chama hicho, Godson Mollel alisema wanalaani vikali tukio la hivi karibuni la kushambuliwa kwa mwenzao mkoani Geita na watu wasiojulikana kwa kinachodaiwa ni imani za kishirikina.
 
“Tunalaani vikali tukio la kuvamiwa na kushambuliwa vikali kwa Kazungu Julius ambaye ni mtoto wa mwenye ualbino mwenye umri wa miaka 10 katika eneo la Mtakuja, Katoro mkoani Geita” alisema Mollel.
 
Mollel alisema wana wasiwasi na kushambuliwa kwa watu wenye ualbino kuhusishwa na imani za kishirikina hasa kuhusiana na shughuli za uchimbaji wa madini ama shughuli za kisiasa.
 
Mratibu wa Dawati la watetezi wenye ulemavu kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Perpetua Senkoro alilitaka Jeshi la Polisi mkoani Geita kuhakikisha watu hao wanakamatwa na kufikishwa Mahakamani.
 
Alisema kuendelea kwa matukio hayo kunatokana na kushindwa kukamatwa kwa watu hao na kuchukuliwa hatua ikawamo kufikishwa mahakamani ili haki itendeke kwa waathirika wa matukio hayo.
 
“Wito wetu kwa Jeshi la Polisi, Serikali na jamii tunaomba kila mmoja afanye kazi kwa weledi katika nafasi yake ili mwisho tusikutane tena hapa kuja kulalamika kuhusu haya matukio” alisema Perpetua.
 
Alisema karne tuliyonayo si ya kujadili masuala ya imani za kishirikina na matukio ya ukatili na udhalilishaji bali ni muda wa kujadili masuala mengine ya maendeleo, hivyo kuendelea kutokea matukio hayo kunarudisha nyuma jitihada za maendeleo nchini.