Kesi hizi za usajili kila mara zinaharibu taswira ya soka

Nipashe
Published at 04:46 PM Apr 16 2024
Nembo ya Fifa.
PICHA: MAKTABA
Nembo ya Fifa.

IMEKUWA ni kama kawaida sasa kila baada ya miezi michache kusikia klabu ya Tanzania imefungiwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kwa kushindwa kumlipa mchezaji, kocha, kukiuka taratibu na kanuni za uhamisho, au ikipewa siku kadhaa iwe imemalizana nao.

Cha kushangaza ni kwamba unaweza kuona klabu inafungiwa kusajili leo, halafu miezi michache tu, inakuja barua nyingine kutoka FIFA, ikiifungia tena timu ile ile kwa mchezaji mwingine, wakati hata bado haijamalizana na mchezaji wa kwanza, mara myingine inaibuka tena.

Ni hivi majuzi tu, Klabu ya Yanga imefungiwa kufanya usajili wa wachezaji wa ndani ya nje kutokana na kesi kama hizo kwa kukiuka kanuni ya za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu, FIFA.

TFF, nayo ikapigilia nyundo, nayo ikaifungia Yanga kufanya usajili kwa wachezaji wa ndani.

Sababu iliyotolewa ni kwamba imekiuka kile kilichoelezwa ni 'Annexe 3', ya Kanuni ya Uhamisho wa Wachezaji (RSTP) ya shirikisho hilo, ambapo haikuingiza uthibitisho wa malipo ya uhamisho wa mchezaji husika ambaye hakutajwa na TFF katika Mfumo wa Usajili (TMS), licha ya kukumbushwa kufanya hivyo.

Inawezekana barua ya FIFA iliyoandikwa kwa TFF imeeleza kila kitu, lakini hadi sasa haijajulikana ni mchezaji gani ambaye alisajiliwa na uthibitisho wa malipo ya uhamisho haikuthibishwa.

 Kwa mujibu wa barua hiyo, Na suala kufikisha kwenye Sekretarieti ya Kamati ya Nidhamu ya FIFA, ina maana kuna adhabu nyingine zaidi itatolewa? Nadhani haya yote mashabiki wa soka wanahitaji kupata majibu ili suala likae sawa, kwa sababu si tu limewachanganya sana wanachama na mashabiki wa Yanga, pia limewashtua.

Kuna kipengele kinachosomeka kuwa Yanga inatakiwa kutekeleza matakwa hayo kikanuni na kuwasilisha taarifa  kwa Sekretarieti ya Kamati ya Nidhamu ya FIFA ambapo suala hilo limefikishwa kwa ajili ya hatua zaidi.

Kwa hapa Tanzania, japo Yanga imekuwa mara kwa mara ina mizozo, lakini klabu nyingi nchini zimekuwa na matatizo kwenye uhamisho, na kuachana na wachezaji na makocha wao kwa usalama bila kudaiana.

Hili limekuwa likilipaka matope nchi yetu na Ligi ya Tanzania ambayo kwa sasa ni ya sita kwa ubora Afrika.

Hali hii inapaswa kuepukwa na kupigwa vita vikali kwani ikiendelea klabu za Tanzania zitakosa uaminifu na kutowapata tena wachezaji bora wa kigeni ambao watakuwa wanaogopa kutotekelezewa matakwa yao, na hata mikataba yao kuvunjwa kiholela na kulazimika kukimbilia FIFA.

Ikumbukwe wachezaji hawa wa kigeni ndiyo wanachangia kwa kiasi kikubwa kulipaisha soka la Tanzania kiasi cha kufanya vema kwa klabu zetu kimataifa.

Tunawashauri viongozi wa klabu za soka nchi kuwa makini sana kwenye mikataba ya makocha wachezaji, uhamisho na vitu vingine vinavyofanana na hivyo, ikiwamo hata kufanya udanganyifu wa nyaraka kwenye mitandao ya uhamisho ya TMS, vinginevyo ipo siku wanaweza kujikuta wanaziingiza klabu zao na hata nchi kwenye matatizo makubwa.

FIFA huwa hawaangalii ukubwa wa timu, hata klabu kubwa barani Ulaya zimekuwa zikipata adhabu, kwa mantiki hiyo ukubwa na sifa ya Tanzania na siasa zetu za mpira wa haziwezi kufanya kazi mpaka huko, zikasamehewa au busara ikatumika.

Tunaamini ushauri huu utafanyiwa kazi kwa mustakabali mpana wa soka la nchini yetu ambalo kwa sasa limepiga hatua kubwa, hivyo hatutarajii kuona linajirudi tena kwa sababu kama hizo.