Wananchi hatari hii mnayoikimbilia mpaka lini?

Nipashe
Published at 04:46 PM Apr 16 2024
Ajali ya lori la mafuta.
PICHA: MAKTABA
Ajali ya lori la mafuta.

KUMEKUWA na kawaida kila inapotokea jambo la hatari wananchi kuwa na kawaida kulimbilia badala ya kujiepusha nalo.

Hili limetokea mara kadhaa, licha ya elimu kutolewa mara kwa mara, lakini bado wananchi wanaonekana kuziba masiko au kujifanya hawaoni.

Askari wa Usalama Barabarani kila mara wanatoa elimu watu kuacha kukimbilia ajali ili kuepusha majanga zaidi yasitokee, lakini wananchi wanaamua kujitoa mhanga.

Miaka kadhaa iliyopita kulitokea ajali ya lori la mafuta na wananchi walikimbilia kuchota mafuta bila kujali hatari inayoweza kuwapata na ajali hiyo ilishuhudiwa watu wengi wakipoteza maisha. Haikupita miaka mingi, ajali nyingine ya lori la mafuta ikatokea mkoani Morogoro na kwa staili ile ile, wananchi wakaikimbilia ili kwenda kuchota mafuta.

Kilichotokea kwenye ajali hiyo kila mtu atakuwa anakumbuka. Watu wengi walipoteza maisha na wengi wakabaki na ulemavu wa maisha.

Serikali imejitahidi kutoa elimu mara kwa mara kuwaonya watu kuacha kukimbilia ajali zinazotokana na malori ya mafuta kwa sababu hatari yake ni kubwa wakati wowote yanaweza kulipuka.

Wakati machungu ya kumbukumbu ya ajali hizo hayajapotea, juzi eneo la Miyomboni, Kata ya Misugusugu, wilayani Kibaha, mkoani Pwani, ilitokea ajali ya lori la mafuta kuacha njia na kupinduka.

Kitendo cha lori hilo kupinduka, kiliwaamsha baadhi ya wananchi wanaoishi eneo hilo na wale wa karibu kwenda kuchota mafuta na kuondoka nayo bila kujali kuwa kuna binadamu wenzao waliokuwa ndani ya lori hilo ambao walikuwa wakihitaji msaada wa kuokolewa.

Kila mmoja alikuwa anakimbilia achote mafuta ili aende kuyauza, hakufikiria kuwa kitendo hicho ni hatari kingeweza kuhatarisha maisha yao.

Cha kumshukuru Mungu ni kwamba ajali hiyo haikuleta madhara kama zilivyotokea ajali nyingine zilizohusisha malori ya mafuta.

Wananchi bado wanahitaji elimu na kukumbushwa kila wakati athari ya kukimbilia ajali kwa sababu wanachoangalia ni namna watakavyopata pesa kutokana na kile wanachokwenda kukichukua.

Gharama inayotokana na ajali kama hizo ni kubwa kuliko hata hiyo pesa wanayokwenda kupata baada ya kuuza mafuta hayo.

Ugumu wa maisha upo, lakini kutoa rehani maisha yako kwa sababu ya shibe ya siku moja ni jambo linalosikitisha.

Ubinadamu umepotea kabisa, inapotokea ajali wananchi wanachojali ni kukimbilia kuiba mali zilizomo ndani ya magari, hata wanapoona binadamu mwenzao akiomba msaada wa kuokolewa wanamuacha apoteze maisha, wanachothamini ni kile watakachokipata kwenye magari hayo.

Kwa ajali iliyotokea juzi huko Pwani, wananchi walionekana kukimbilia kuchota mafuta wakiwa wamerundikana kila mmoja akiwa amebeba dumu analoona linafaa kubeba mafuta hayo bila kujihurumia.

Kinachosikitisha zaidi inapotokea ajali kama hizo watoto nao hukimbilia na wengine wazazi wao kuwahamasisha kwenda nao ili waweze kupata mafuta mengi zaidi.

Kwa ajali hiyo ya Mkoa wa Pwani, imeelezwa kuwa watu sita wameshakamatwa kwa kuhusika kuchota mafuta na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo, amethibitisha kuwa hakuna madhara ya kibinadamu yaliyotokea.

Kwa hilo la kutotokea madhara kwa binadamu ni la kumshukuru Mungu, vinginevyo tungekuwa kwenye msiba mwingine wa kupoteza watu kwa kuungua na mafuta.

Wananchi jiepusheni na kukimbilia majanga, nguvu kazi kubwa inapotea.