Azam, Mashujaa vita kali vya malengo leo

By Saada Akida , Nipashe
Published at 06:57 AM Apr 17 2024
news
Picha: Azam FC
Kocha Mkuu wa Azam FC, Bruno Ferry, akiwa na Kocha msaadizi Youssouph Dabo.

AZAM FC leo inashuka dimbani kukabiliana na wegeni wao, Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam huku kila moja ikipigania malengo yake, moja ikitaka kumaliza nafasi ya pili na nyingine kujinusuru kushuka daraja.

Timu hizo zinakutana kwa mara ya pili, baada ya mwaka jana kukutana kwenye mzunguko wa kwanza ambapo Mashujaa FC wakiwa nyumbani walikubali kichapo cha mabao 3-0 katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma. 

Azam FC itashuka dimbani ikitoka kupata ushindi ugenini dhidi ya Namungo FC, kwenye mechi iliyopigwa Uwanja wa Majaliwa,  Ruangwa mkoani Lindi wakati Mashujaa FC wenyewe wakitoka kupoteza mechi nyumbani dhidi ya Coastal Union.

Kuelekea mchezo huo Kocha Mkuu wa Azam FC, Bruno Ferry, amesema wamejiandaa vizuri kwa mchezo wao wa leo dhidi ya Mashujaa baada ya kutoka kufanya vizuri dhidi ya Namungo FC. 

Alisema mchezo huo ni muhimu kwao kutafuta pointi tatu kwa sababu wako kwenye vita vya kuwania nafasi ya pili na Simba, hivyo wakipoteza mechi hiyo watakuwa katika kipindi kigumu.

“Hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu wapinzani hawako nafasi nzuri na wametoka kupoteza, tutacheza kwa tahadhari kubwa na umakini ili kutafuta alama tatu dhidi ya Mashujaa FC, “ alisema Ferry.

Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Mohammed Abdallah ‘Bares’,  alisema wanakabiliwa na mechi ngumu na wanaingia kwa tahadhari kubwa ya kutafuta matokeo chanya dhidi ya Azam FC.

Alisema mchezo wa leo maana yake kubwa ni kutafuta matoke kwa sababu hali ya Mashujaa FC haiko katika nafasi nzuri na kulazimika kutafuta matokeo chanya. 

“Hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu ukiangalia timu zote kila moja imekuwa na malengo yake kwa upande wetu kujiondoa katika nafasi ya chini, ambayo tupo kwa sasa,” alisema Bares.