Azam yaiweka pabaya Simba michuano ya CAF

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:28 AM Apr 16 2024
news
Picha: Azam FC
Kocha wa Azam FC, Youssoph Dabo.

USHINDI wa mabao 2-0 ilioupata juzi usiku dhidi ya Namungo FC, kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi, umeifanya Azam FC kung'ang'ania nafasi ya pili, ikifikisha pointi 50 na kuiweka njia panda Simba kwenye ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Azam imenufaika na sare ya bao 1-1 ambayo Simba iliipata Jumamosi iliyopita dhidi ya Ihefu, ambapo sasa imekaa kwenye nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi nne, ingawa ipo mbele michezo miwili zaidi ya Wekundu wa Msimbazi hao wanaosuasua, ambao wana mechi ngumu dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga, Jumamosi wiki hii.

Mabao yote ya Azam yalifungwa na Kipre Junior dakika ya 62 na 84, na kuifanya timu yake si tu kwamba imeongeza pointi tatu, lakini pia imelipa kisasi cha kufungwa mabao 3-1 katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa, Oktoba 27, mwaka jana.

Kocha wa Azam FC, Youssoph Dabo, ameeleza kufurahishwa kwake na ushindi huo, akisema kama wakiendelea hivi, basi msimu huu wanaweza kutwaa ubingwa, au kushika nafasi ya pili na kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

"Tumeshinda dhidi ya mpinzani mgumu, tulijitahidi kuwadhibiti tangu kipindi cha kwanza, taratibu tukaanza kuushika mchezo, mwanzo wapinzani walikuwa na nguvu kubwa kwa sababu walikuwa wancheza nyumbani kwao, na kwa sababu walitufunga mzunguko wa kwanza, walitaka kutufunga tena, niliwaambia wachezaji wangu kuwa huu ndiyo wakati, msimu huu tuna nafasi kubwa ya kupata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa kwa msimu ujao, nina furaha sana mimi nawapongeza wachezaji wangu kwa ushindi huu wa ugenini," alisema kocha huyo.

Iwapo Azam itafanya vema katika mechi zake zinazobaki na Simba ambayo ipo kwenye nafasi ya tatu itaendelea kusuasua, basi inaweza kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao, na kuiacha Simba ikienda kucheza Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Wakati Azam ikiwa imecheza mechi 22 na kujikusanyia pointi 50, Simba imecheza mechi 20, na kuvuna pointi 46, ambapo kwa mwenendo wa ligi unavyokwenda timu hizi mbili zinaonekana kuwania zaidi nafasi ya pili ambayo inatoa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.