Serikali kuunga mkono juhudi soka la vijana

By Saada Akida , Nipashe
Published at 09:18 AM Apr 16 2024
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, akipiga danadana.
Picha: Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, akipiga danadana.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amesema kuwa serikali kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka nchini (TFF), haitakubali kuona juhudi zinazoletwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulimwenguni (FIFA), katika maendeleo ya soka la vijana nchini kuanzia ngazi ya chini zikitoweka.

Kauli hiyo aliitoa jana katika uzinduzi wa program ya mpira wa miguu kwa ajili ya watoto kwenye shuleni iliyoandaliwa na TFF kwa kushirikiana na FIFA na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwa ajili ya mafunzo kwa walimu 46 wa  shuleni za msingi kutoka wilaya 16 nchini.

Msigwa alisema walimu waliopata mafunzo hayo wanatakiwa kuzingatia kwa sababu hiyo ni fursa ambayo imepata nchini kwa kutoa elimu shuleni ili ujuzi huo waupate watoto.

Alisema program hiyo imekuja kimkakati kwa sababu nchini imewekeza katika michezo na kuanzia chini hana budi kuipongeza TFF kuwa karibu na uhusiano mzuri na Fifa na CAF. 

“Kwa sasa hatutalala na kukubali kuona juhudu hizi zinapotea, kwa sababu TFF wanafanya kazi nzuri na ushirikiano mkubwa wa FIFA na CAF, walimu waliopata program hizi wahakikishe wanawatengeneza vijana vizuri 

"Program hii ya mpira shuleni ni kitu muhimu sana kwa sabahu kuna vipaji vingi, lakini hawapati nafasi ila hii inaweza kusaidi kwa taifa letu kwa siku za mbele,” alisema Msigwa.

Aliongeza kuwa nchini itakuwa wenyeji wa AFCON 2027, hivyo kunatakiwa kuwa na maandalizi makubwa ikiwamo kuandaa timu za taifa na inaanzia shuleni, kitu ambacho walimu wanatakiwa kutumia vizuri mifumo hiyo maalum kuwapika vijana wa kesho.

Naye Meneja wa program hiyo wa Fifa, Antonio Sanchez, alisema program hiyo ni maalum kwa vijana hao na inafaida kubwa kwani mbali na soka mtoto pia atapata elimu ya kujifunza vitu vingine zaidi.