Yanga SC, Aziz Ki wanoga Kileleni

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:36 AM Apr 15 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Stephane Aziz Ki (mgongoni), akimpongeza Joseph Guede na kushangilia naye baada ya kuifungia Yanga bao la kwanza dhidi ya Singida FG, kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa CCM Kirumba jana. Yanga ilishinda mabao 3-0.

MABAO mawili ya Muivory Coast, Joseph Guede na moja la Mburkina Faso, Stephane Aziz Ki, jana yaliwapa Mabingwa Watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Singida Fountain Gate na kuiongezea mbio za ubingwa.

Lakini pia ushindi huo ni ishara ya salamu kwa watani zao wa jadi, Simba watakaokwenda kukutana nao Jumamosi ijayo, Uwanja wa Benjemin Mkapa, Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, ilishuhudia Clement Mzize akitoa pasi mbili za mabao 'asisti', huku Aziz Ki akiongeza bao moja na kufikisha 14, akikaa kileleni mwa orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu na kumuacha Feisal Salum, 'Fei Toto' mwenye mabao 13.

Haikuwa mechi yenye ufundi sana kutokana na uwanja kuwa na matope na maji yaliotuama kwenye maeneo mengi uwanjani, kiasi cha kusababisha wachezaji kucheza kwa wanavyojua wao, lakini si kwa kutumia mifumo ya makocha wao.

Wachezaji wa timu zote mbili walionekana wakiteleza na kuanguka wanapokimbilia mpira, au wanapopigwa chenga.

Dakika ya kwanza tu, Yanga ilianza kulitia msukosuko lango la Singida Fountain Gate dakika ya kwanza tu, wakati Clement Mzize alipotanguliziwa mpira kwa Jonas Mkude, lakini akiwa ana kwa ana na kipa Benedict Haule, shuti lake lilitoka nje.

Nicolaus Gyan, mchezaji wa zamani wa Simba, alijibu shambulizi hilo dakika ya pili kwa shuti kali nje ya eneo la hatari, lakini mpira ukapaa juu ya lango.

Haule, alifanya kazi ya ziada kwa timu yake, alipotema shuti kali la Maxi Nzengeli alilolipiga akiwa ndani ya boksi, na mpira huo kwa sababu ulikuwa na nguvu bado ulikuwa unaelekea wavuni, lakini aliurukia na kuudaka ukiwa haujavuka mstari wa lango.

Kwa mara nyingine tena, Mzize aliikosesha Yanga bao dakika ya 33, alipounganisha kichwa ambacho hakikulenga lango, alipoletewa pasi ya juu na Nzengeli.

Yanga ilifanikiwa kuandika bao dakika ya 41, lililofungwa na straika Guede, raia wa Ivory Coast, aliyesajiliwa kipindi cha dirisha dogo.

Aliupata mpira mrefu iliopigwa kutoka katikati ya uwanja, na akiwa pembeni kwenye wingi ya kushoto, alimpindua nahodha wa Singida Fountain Gate,  Biemez Carno, raia wa Jamhuri ya Kidemkorasi ya Congo, akapiga shuti lililombabatiza kichwani beki, Idd Habib, mpira ukampoteza maboya kipa Haule, na kujaa wavuni.

Bao la pili la Yanga liliwekwa wavuni na Aziz Ki dakika ya 65 kwa shuti kali la mbali kiasi cha mita 30 kwa mguu wa kushoto ambalo lilimkuta kipa Haule akiwa hajajiandaa na kujaa wavuni.

Dakika tatu baadaye, Guede alipachika bao la tatu kwa Yanga na la pili kwake kwa kichwa maridadi, baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Mzize.

Kazi kubwa ilianza kufanywa na mfungaji mwenyewe alipata mpira toka nyuma kwa Khalid Aucho, akakimbia nao umbali mrefu, kabla ya kumpa Mzize ambaye alimuacha mfungaji kukaa kwenye eneo zuri na kumrudishia mpira.

Yanga imefikisha pointi 55 kwa michezo 21 iliyocheza, ikiendelea kupunga hewa kileleni mwa msimamo, huku Singida Fountain Gate ikishuka kutoka nafasi ya nane hadi ya tisa, ikibaki na pointi zake 24, ikiwa imecheza mechi 22.