Yanga yaonya mashabiki 'dabi' Simba Jumamosi

By Saada Akida , Nipashe
Published at 09:05 AM Apr 16 2024
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe.

MSEMAJI wa Yanga, Ali Kamwe, amesema licha ya Simba kupitia kipindi kigumu cha kutopata matokeo mazuri, lakini wanaitazama timu hiyo katika mambo matatu muhimu kuelekea mchezo wa Derby utakaopigwa Jumamosi wiki hii.

Kikosi cha Yanga kilirejea jana kutoka jijini Mwanza kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Fountain Gate ambayo kilishinda mabao 3-0, na leo kinaingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo wa Kariakoo 'Derby', ambao utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam saa 11:00 jioni.

Akizungumza na Nipashe jana, Kamwe alisema anewataka mashabiki kuachana na fikra ya kuwa mpinzani wao amechoka na hajapata matokeo mazuri bali wanatakiwa kufikiria namna ya kuzipata pointi tatu mbele ya Simba.

Alisema mechi ya Simba na Yanga ina umuhimu wake, na kwamba haitakiwi kwenda uwanjani na mawazo ya pointi tatu kwa kufikiri mpinzania wao amechoka, jambo ambalo wanatakiwa kuliondoa kichwani na kutambua wanaenda kukutana na timu tishio.

“Hatuitazamani Simba kama wanavyotazama mashabiki, bali kwetu ni timu tishio na tuko nao katika vita, kwa sababu wana wachezaji wazoefu kwenye kucheza Derby kubwa na tofauti pia viongozi makini na wenye mipango na ubora wa hizi mechi,” alisema Kamwe.

Aliwataka mashabiki wa Yanga, kuwa kujitokeza uwanjani na kuifanya Kariakoo Derby kuwa kama Kilele cha Siku ya Wananchi kwa kujaza uwanja na kutowapa nafasi ya wapinzani wao kuwa wengi.

“Asitokee Mwanayanga akabaki nyumbani na baada ya matokeo akajisifia, tunahitaji siku hizo kuwa ni Kilele cha Siku ya Wananchi na tusiwape nafasi mashabiki wa upande wa pili kuwa wengi,” alisema Kamwe.

Kuhusu majeruhi, alisema baadhi ya wachezaji wamerejea akiwamo Kennedy Musonda na Pacome Zouzoua yuko katika hatua nzuri ya kurejea katika hali yake ya kwaida.

“Hatuwezi kuwalazimisha wachezaji kucheza kwa sababu Yang ina kikosi kipana na tunaenda siku hiyo kwa roho ya kikatili,” alisema Kamwe.

Katika hatua nyingine  Yanga kwa kushirikiana na Benki ya NBC, wamezindua kadi ya wanachama wa klabu hiyo ambayo itawasaidia katika mambo mbalimbali ikiwamo kuingia uwanjani.

Kwa munibu wa rais wa Yanga, Mhandisi Hersi Said, alisema Yanga inajivunia  kuingia makubaliano na Benki bora ya NBC kwenda kuwahudumia wanachama wao kwenye usajili na kutoa kadi za uanachama.

Alisema ukijiunga kuwa mwanachama wa Yanga, hapo hapo utapata huduma za kibenki, lakini kubwa zaidi kadi ya NBC imeungajishwa na huduma za N-CARD, hivyo mwanachama wa Yanga atapata huduma ya kuingia uwanjani pamoja na huduma za usafiri.