Marekani, IRDP kuendelea kutokomeza umaskini

By Valentine Oforo , Nipashe
Published at 09:51 AM May 10 2024
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle.
Picha: Mtandaoni
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle.

BALOZI wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle amesema Serikali ya Marekani itaendelea kuimarisha uhusiano wa kikazi na Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) ili kuunga mkono jitihada za Tanzania katika kutokomeza umaskini.

Aliyasema hayo juzi alipofanya ziara maalum katika chuo hicho jijini hapa yenye lengo la kujionea namna vijana wanavyofundishwa ujuzi mbalimbali za kibiashara na kibunifu.

Alionesha kufurahishwa na programu mbalimbali za mafunzo ya ujasiriamali na ubunifu zinazoanzishwa na kufadhiliwa na Marekani chuoni hapo kwa lengo la kuwakomboa vijana kiuchumi. 

Alisema kwa miaka saba sasa Ubalozi wa Marekani na chuo hicho wamekuwa wakishirikiana katika kutekeleza programu mbalimbali za mafunzo zinazolenga kuwainua vijana kiuchumi.

Ofisa wa Masuala ya Utamaduni, Sehemu ya Masuala ya Umma katika Ubalozi wa Marekani, Chad Morris, alisema:  “Sisi katika ubalozi tunajivunia sana kwa uhusiano ambao tumejenga na IRDP kwa miaka saba iliyopita, kumekuwa na utekelezaji wa kitaalamu mradi wetu wa ujasiriamali kwa wanawake." 

Morris alisema ubalozi huo unatafuta njia zaidi za kuendeleza na kutekeleza programu muhimu zaidi katika chuo hicho cha serikali, hasa programu zinazolenga kuwawezesha vijana.

Mkuu wa chuo hicho, Prof. Hozen Mayaya alisema ziara ya Balozi Battle ni ishara njema ya mwendelezo wa ushirikiano baina ya pande hizo mbili.

Alisema: "Uhusiano wetu wa kikazi na Ubalozi wa Marekani umedumu kwa miaka saba sasa na kupitia ushirikiano huu wa muda mrefu tumeona na kupata mafanikio mengi,”

Aliitaja baadhi ya miradi ambayo chuo imefanikiwa kuutekeleza kwa ushirikiano na Ubalozi wa Marekani kuwa ni mradi wa  'Academy for Women in Entrepreneurship (AWE), pamoja na Mipango Entrepreneurship and Innovation (MEI) ambayo yote imejikita katika kuwawezesha vijana.

Naibu Mkuu Taaluma wa chuo hicho, Prof. Provident Dimoso, alisema kupitia uhusiano huo na Ubalozi wa Marekani, chuo kimefanikiwa kujenga ushirikiano mzuri na vyuo vikuu mbalimbali vikubwa nchini Marekani.