SMZ, UNESCO kulikarabati jengo la sinema Majestic

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 10:03 AM May 10 2024
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhammed Mussa.
Picha: Mtandaoni
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhammed Mussa.

SERIKALI ya Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), wanatarajia kulifanyia ukarabati jengo la sinema majestic lililoko katika Hifadhi ya Mji Mkongwe.

Hatua hiyo inalenga kulifanya jengo hilo kuwa kituo kikuu cha utamaduni visiwani hapa.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Muhammed Mussa, aliyasema hayo juzi wakati akifungua warsha ya kujadili mikakati ya ukarabati wa jengo hilo iliyoshirikisha timu ya wataalamu kutoka UNESCO, Japan, Saudi Arabia na Hifadhi ya Mji Mkongwe.

Alisema serikali ina mikakati ya kuhakikisha majengo yote ya Mji Mkongwe yanafanyiwa ukarabati na kurejesha haiba na taswira ya awali.

Leila alisema kukamilika kwa ukarabati huo, kutaongeza vivutio vya utalii nchini na nchi kuendelea kupata watalii wengi zaidi ambao baadhi ya watalii wanaofika visiwani hapa hupenda kujifunza historia.

Aidha, alisema zoezi hilo limelenga kuliboresha jengo hilo lenye historia kubwa na kuendelea kuupa hadhi ya urithi wa dunia.

Alisema mbali ya maonesho ya sinema, ujenzi huo utakapokamilika, litatumika kwa matukio mbalimbali ya kitamaduni, zikiwamo ngoma na filamu za asili, kurekodi kazi za wasanii na kutoa burudani nyingine za kijamii zitakazovutia watalii na wananchi.

Naye Mwakilishi wa UNESCO nchini Tanzania, Michel Toto, alisema shirika hilo litaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika mambo mbalimbali yakiwemo ya utamaduni kwa maslahi ya sasa na kizazi kijacho.

Mkurugenzi wa Taasisi ya ‘Hifadhi Zanzibar’ inayoshirikiana na UNESCO kufanikisha mradi huo, Tolnino Sarav, alisema watahakikisha kazi ya kulifufua jengo hilo inafanyika kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Jengo la sinema Majestic lilijengwa zaidi ya miaka 100 iliyopita, na ukarabati wake unahitaji Dola za Marekani milioni moja hadi kukamilika kwake.

Wadau mbalimbali walioshiriki warsha hiyo, walisifu hatua ya Serikali ya Zanzibar na UNESCO kuja na mradi huo, wakisema una umuhimu mkubwa na jengo hilo ni miongoni mwa vyanzo vya mapato.