Tindikali ya chini katika udongo chanzo uzalishaji mdogo

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 10:45 AM Apr 30 2024
Tindikali ya chini katika udongo.
Picha: Maktaba
Tindikali ya chini katika udongo.

MIKOA yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula ikiwemo ya Nyanda za Juu Kusini, imetajwa kuwa na udongo wenye tindikali ya chini, hali inayosababisha wakulima watumie gharama kubwa kwenye uzalishaji na wasipate tija.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Idara ya Masoko na Mauzo wa kampuni ya mbolea ya Minjingu, Dk. Mshindo Msola kwenye mafunzo kuhusu usimamizi wa rutuba ya udongo na matumizi bora ya mbolea kwa mawakala wa pembejeo za kilimo kutoka mikoa ya Njombe, Morogoro, Iringa,na Ruvuma yaliyofanyika mjini Makambako.

Alisema kutokana na mikoa hiyo kuwa na udongo wenye tindikali ya chini wakulima wanatakiwa kutumia chokaa kilimo ili kukabiliana na hali hiyo.

Dk. Msola alisema kutokana na changamoto hiyo serikali kupitia wizara ya kilimo licha ya kutoa mbolea za ruzuku pia inatakiwa kutoa ruzuku ya chokaa kilimo ili kuwawezesha wakulima kuboresha hali ya udongo ambao utawasaidia wazalishe kwa tija.

“Kwenye mikoa mingi yenye uwezo wa kuzalisha nyanda za juu kusini milimani, Kanda ya Ziwa, upande wa Kigoma baadhi ya maeneo upande wa Kilimanjaro udongo unatindikali ya chini ya 5.5 sasa madhara yake ukishakuwa na udongo wa tindikali hii ni lazima uutibu,” alisema Dk. Msola.

Dk. Msola alisema kuwa tindikali ikiwa ya chini maana yake kuna madini ambayo yako kwa wingi ambayo yanaitwa aluminium na chuma.

“Madini haya ni kama minyoo kwenye ardhi kwa hiyo kadri unavyoweka mbolea inakamata yenyewe na mbolea haipatikani kwa hiyo ushauri wangu kwanza wakulima washauriwe watumie chokaa kilimo ambayo itawasaidia na mashamba mengi yatafufuka,” alisema Dk. Msola.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka alitoa rai kwa maofisa kilimo kutumia utafiti huo kuona namna ya kukabiliana na changamoto ya udongo kuwa na tindikali ya chini ili kuhakikisha kutatua changamoto hiyo na kuwasaidia wakulima wazalishe mazao bora.

Baadhi ya mawakala wa pembejeo za kilimo akiwemo Lesa Mbilinyi alisema watahakikisha wanatoa elimu kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya pembejeo hasa mbolea na mbegu ili wazalishe kwa tija. 

Awali akizungumza katika mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa alisema iko haja ya kuboresha ardhi ili wakulima wazalishe kwa tija na wameiomba serikali kuona namna ya kupunguza gharama za chokaa kilimo.