Ukuaji sekta ya utalii kwa wavutia wanasayansi, w’biashara kimataifa

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 09:25 AM May 10 2024
Mbungani.
Picha: Mtandaoni
Mbungani.

KASI ya ukuaji wa sekta ya utalii nchini imeanza kuwavutia wanasayansi na wafanyabiashara wa kimataifa kulipigia chapuo, Shirika la Hifadhi za Taifa ‘TANAPA, Jumuiya ya Waongozaji wa Utalii na Mawakala wa Utalii kutoyakwepa maendeleo ya kidijitali.

Badala yake wameshauri ili kuepusha matukio ya ujangili wa wanyamapori, watalii kupoteana na waongoza utalii na kuwasaidia mawakala wa utalii kujua wageni wamefika kituo gani na kama wako salama, hawawezi kuepuka matumizi ya teknolojia ya QR Codes Track (misimbo milia) kama zinavyofanya nchi nyingine duniani.

Jana, mwanasayansi kutoka Singapore, Rangesh Nallan, ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Digiticket Afrika, alisema rekodi ya Tanzania kupokea watalii milioni 1.8, sawa na asilimia 118 kwa mwaka jana, ikiwa ni ongezeko la asilimia 32 kabla ya ugonjwa wa UVIKO-19, inapaswa kwenda sambamba na uwekezaji wa maendeleo ya dijitali ya misimbo milia ili kuvutia watalii wengi duniani.

“Tanzania sasa inapaswa kuiga mataifa mengine yanayoendesha sekta ya utalii kwa mafanikio kama Afrika ya Kusini, ambayo inatumia huduma ya misimbo milia kwa watalii wanaoingia kwao,” alisema. 

Akizungumzia teknolojia hiyo, mwongozaji wa utalii, Hollyfield Mbona, alisema ujio wa teknolojia hiyo ya misimbo milia, ni moja ya utatuzi wa changamoto kubwa ya Tanzania, kukabiliana na ongezeko la kasi ya watalii, baada ya Filamu ya ‘The Royal Tour’ iliyotengenezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mkurugenzi wa SkyNet Solutions, Epifan Benard, alisema wameingia makubaliano ya kufanya kazi na kampuni ya QR Codes 4you ya nchini Singapore, ambayo inataka kutoa huduma hiyo ya misimbo milia kwenye sekta ya utalii nchini.

Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, mwaka 2023, watalii waliongezeka kutoka nchi za Marekani kwa asilimia 16, Italia asilimia 8, Canada 7.6, Uingereza 5.9 na Ufaransa 5.4.

Wakati watalii kutoka nchi za Afrika, waliongezeka kutoka nchi za Zambia, Kenya, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Aidha, alisema mapato ya nchi kupitia sekta ya utalii, yameongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 3.5 hadi Dola za Marekani 3.4 ikiwa na ongezeko la Dola za Marekani bilioni 1.5

Kairuki, alisema serikali inaendelea na juhudi za kutangaza zaidi utalii ili kupata watalii wengi kutoka katika nchi za China, India, Urabuni na Amerika ya Kusini.